Kichapo cha mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Biashara United Mara kimemuibua Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Ruvu Shooting Masau Bwire kwa kumuangushia lawama mwamuzi Martin Saanya.

Masau ambaye alikua shuhuda wa kichapo hicho kilichotolewa jana Jumapili (Februari 21) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma, Mara  amesema mwamuzi saanya hakuwatendea haki kwa kutoa mkwaju wa Penati, uliowapa nafasi ya kuongoza Biashara United Mara.

Amesema maamuzi ya Saanya hayakuwa sahihi, na anaamini mkwaju wa Penati walioupata wenyeji wao kipindi cha kwanza uliwatoa mchezoni wachezaji wa Ruvu Shooting waliokua na matumaini makubwa ya kushinda ugenini.

“Hamna namna kwetu sisi kuonekana tumeshinda ama tumepoteza ila ukweli ni kwamba baada ya ile penalti naona kabisa ari ya wachezaji ilipungua.”

“Kweli walitolewa mchezoni kwa ajili ya suala hilo hivyo ninawaomba mashabiki waamini kwamba timu yetu ipo imara na itaendelea kupambana kufikia malengo tuliyojiwekea.” Amesema Masau .

Mwamuzi Martin Saanya aliizawadia Biashara United Mara mkwaju wa Penati, dakika ya 34 kwa madai mchezaji wa Ruvu Shooting Casian Ponera aliunawa mpira kwenye eneo la hatari, lakini picha za marejeo za televisheni zilionyesha mpira ulimgonga usoni.

Penati hiyo ilipachikwa wavuni na mshambuliaji kutoka nchini Ghana Christian Zigah dakika ya 36.

Mabao mengine ya Biashara United Mara kwenye mchezo huo yalifungwa na Lenny Kissu dakika ya 45 na Yusuph Athuman dakika ya 68.

Kwa ushindi huo Biashara United Mara imefiksha alama 35 na kuendelea kusalia katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku Ruvu Shooting wakishuka nafasi moja kutoka nafasi ya tano hadi ya sita, kwa kuendelea kuwa na alama 31 sawa na KMC FC, wenye mabao mengi ya kufunga.

Namungo FC yapangwa na Waarabu
Kaze amkingia kifua Sarpong