Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomez Da Rossa amesema atahakikisha kikosi chake kinapambana vilivyo dhidi ya Tanzania Prisons ili kupata alama tatu muhimu.
Simba SC leo itakua mwenyeji wa Maafande hao wa Jeshi la Magereza kutoka mkoani Rukwa mjini Sumbawanga, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa moja jioni.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amesena kushinda dhidi ya Tanzania Prinsons kutaendelea kuongeza chachu ya kutetea taji la Tanzania Bara, huku wakiipa Presha Young Aficans inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu.
“Kwa sasa akili yetu ni juu ya mchezo wetu dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo huu ni muhimu kwetu kwa sababu tunataka kuwapa presha Young Africans ambao wapo juu yetu.“
“Tukishinda tutakuwa karibu yao zaidi na hii itakuwa nzuri kwetu, muhimu tutacheza tukiwa tunajua ni kitu gani ambacho tutakuwa tunakitaka.” Amesema kocha Didier.
Mchezo wa leo unachukuliwa kama kisasi kwa Simba SC baada ya kupoteza mbele ya Tanzania Prisons kwa 1-0, kwenye mzunguuko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumiliki alama 45, huku Tanzania Prisons wakiwa kwenye nafasi ya 10 kwa kuwa na alama 29.