Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewaonya mafundi wa simu za mkononi wanaofuta namba za utambulisho wa simu (Imei) za simu za wateja akisema kitendo hicho ni kinyume cha sheria.
Ndugulile ametoa onyo hilo katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Arusha, ambapo amezungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mkoani humo.
Amesema kufuta namba hizo ili simu zitumike tena ni kosa la kisheria na Serikali itawachukulia hatua kali mafundi hao kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.
Waziri Ndugulile ameyasema hayo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa TCRA, Imelda Salum kuhusu mafunzo maalumu yaliyotolewa kwa mafundi simu 332 wa kanda hiyo inayojumuisha mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
Katika hatua nyingine Dk Ndugulile ameielekeza TCRA kuangalia namna ya kupunguza gharama za usajili na utoaji leseni kwa wamiliki wa Runinga za mtandaoni (Online TV), kwa kuwa eneo hili linawapatia vijana wengi ajira na gharama za usajili na leseni ni kubwa.
Pia, ameielekeza TCRA wapunguze muda walioweka wa kuendelea kusajili wamiliki hao kwa kuwa mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ni mbali.