Mkoa wa Kagera umeungana na Mikoa  mingine nchini katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji kwa kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa  na serikali pamoja na kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji ambapo wananchi wameaswa kulinda vyanzo hivyo.

Katika taarifa iliyotolewa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Warioba Sanya imeeleza kuwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, Mkoa wa Kagera umeweza kutekeleza miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 263 ambayo haijawahi kutokea kwenye awamu zote za uongozi.

Mhandisi sanya amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano wamewea kujenga miradi ya maji 70 vijijini ambayo tayari imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi, huku miradi 65 ikiendelea kujengwa huko vijiji ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa ukaribu.

DCIM\100MEDIA\DJI_0243.JPG

“Wakati tunaadhimisha hii wiki ya maji sisi kama Wahandisi wa Mkoa wa Kagera tunajivunia kutekeleza miradi mikubwa na yenye tija kwa wananchi wetu, tangu kuumbwa kwa dunia hii uwekezaji mkubwa tena kwenye sekta ya maji haujawahi kufanyika hivyo tunaungana na wananchi wa Mkoa wa Kagera kuishukuru serikali kwa hili,” ameeleza Mhandisi Sanya.

Sanya ameongeza kuwa wao kama wataalamu hawatakuwa sababu ya kukwamisha upatikanaji wa maji kwa wananchi badala yake watahakikisha wananchi wa Kagera wanapata maji safi na salama na yenye kutosheleza kwa kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maji kwa ubora unaotakiwa.

Kuhusu suala la uharibifu wa miundombinu  ya maji, Mhandisi Sanya amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wananchi ambao sio wazalendo na wamekuwa wakihujumu miundombinu ya maji, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara na kuleta usumbufu wa kutopatikana kwa huduma ya maji kwa wananchi wengine, huku akiongeza kuwa kutokana na sheria ya maji wamekuwa  wakiwachukulia hatu wale wote waliokuwa wakibainika.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Kadole Kilugara amesema kuwa  Serikali haitamuonea haya mwananchi yeyote atakayebainika kuhujumu miundombinu ya maji kwa sababu zozote, na kuwataka Wananchi kuwa walinzi namba moja wa miradi ya maji kwakuwa miradi hiyo ni yao.

Akiongea kwaniaba ya wananchi watumia maji wa kijiji cha Rubale, Aishati Saidi ameishukuru Serikali kwa kufufua miradi ya maji iliyokuwa imekufa kwa kipindi kirefu na sasa inatoa huduma ya maji, hivyo kuwapunguzia aadha ya kuhangaika kutafuta maji.

Kaulimbiu ya  wiki ya maji ni “Thamani ya maji kwa uhai na maendeleo”

Tanzia: Rais John Pombe Magufuli afariki dunia, taifa lamlilia
Ndugulile awaonya mafundi simu ufutaji wa Imei namba