Kikosi cha Maafande wa Jeshi la Magereza *Tanzania Prisons* jana Jumanne (Machi 30) kilirejea kambini, tayari kwa maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC).
Tanzania Prisons ambayo msimu huu ina matokeo mazuri katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, bado ipo chini ya kocha msaidizi Shaban Kazumba, akimsaidia Kocha Mkuu Salum Mayanga anayekabiliwa na changamoto za kifamilia.
Kocha Kazumba amesema wachezaji wote wamefika kambini na wameshaanza maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu, huku akiamini wataendelea kupata matokeo kama ilivyokua kabla ya Ligi Kuu kusimama, kupisha maandalizi ya timu ya Taifa *Taifa Stars* na maombolezo ya kifo cha aliyekua Rais wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli.
Amesema wakati wakiangalia namna ya kuendeleza ushindi katika michezo ya Ligi Kuu, pia wameutazama mchezo wa Kombe la Shirikisho (ASFC), utakaowakutanisha na Young Africans, Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Amesema mchezo dhidi ya Young Africans waliufahamu baada ya ratiba ya ASFC kupangwa, na hawana budi kuupangia mikakati ya ushindi ili kuweza kuwa sehemu ya timu zitakazosonga mbele kwenye michuano ya ASFC.
“Tunajipanga kuendelea pale tulipoishia, dhamira yetu ni kuona tunafikia lengo hadi mwishoni mwa msimu huu, hivyo tumeingia kambini kujiandaa na In Shaa Allah tutafanikiwa.”
“Michezo yetu yote ni muhimu, tunaangalia upande wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, hivyo kila upande tunahitaji kufanya vizuri.” Amesema Kazumba
Kocha huyo ameongeza pamoja na matokeo mazuri waliyonayo lakini hawawezi kuridhika isipokuwa lazima waweke mipango sawa ili kuendeleza rekodi nzuri na kumaliza nafasi nne za juu.
“Hata sisi tunatamani zile nafasi tatu za juu ili ikitokea fursa ya kuwakilisha kimataifa tunaenda, kwa sasa timu zimejipanga kujinusuru kushuka daraja kwa hiyo lazima Prisons tuwe makini,” ameongeza Kazumba.
Tanzania Prisons wataendelea na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kucheza dhidi ya Dodoma jiji April 10, mjini Sumbawanga mkoani Rukwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela.
Mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya young Africans utacheza kwenye Uwanja huo kati ya April 30 hadi Mei 02, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo Jumatano (Machi 31) na Bodi ya Ligi Kuu *TPLB*.
Tanzania Prisons inashika nafasi ya 8 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kujikusanyia alama 31.