Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women) Dkt. Phumzile Mlambo-Ngcuka.
Wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Dkt. Phumzile amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyounga mkono juhudi za kupigania masuala ya Wanawake na ameahidi kuwa UN-Women itamuunga mkono katika juhudi hizo.
Amemualika kushiriki katika mkutano utakaojadili masuala ya jinsia uliopangwa kufanyika tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu huko Paris – Ufaransa ambao madhumuni yake ni kuchagiza usawa wa kijinsia kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 baada ya kuonekana baadhi ya maazimio hayajatekelezwa ipasavyo.
Kuelekea mkutano huo, nchi zitakazoshiriki zimegawanywa katika maeneo sita ya kufanyia kazi, na Rais Samia Suluhu Hassan amekubali kuwa kiongozi katika eneo la haki za kiuchumi.
Aidha, Dkt. Phumzile ameeleza kufurahishwa kwake na sekta binafsi ya Tanzania ambayo imekubali kushirikiana na Serikali kusaidia juhudi za kuleta usawa wa kijinsia katika masuala ya kiuchumi kwa Wanawake.
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ameipongeza UN-Women kwa juhudi kubwa za kupigania masuala ya Wanawake ikiwemo maazimio ya Beijing na ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kuungana na UN-Women katika kuongeza msukumo wa utekelezaji wake.
Amebainisha kuwa japo Tanzania bado haijafikia kiwango cha usawa wa kijinsia cha 50/50 katika uongozi, katika kipindi chake atahakikisha anaongeza jitihada za kufikia usawa huo.
Rais Samia Suluhu Hassan ameishukuru UN-Women kwa utayari wake wa kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa corona.