Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), wanakutana leo Jumapili nchini Ghana kujadili mzozo wa kisiasa unaoendelea nchini Mali.
Viongozi hao wataamua kuhusu hatua ya kuchukua kufuatia mapinduzi ya pili katika kipindi cha miezi 9. Kiongozi wa kijeshi wa Mali Kanali Assimi Goita alialikwa kuhudhuria kikao cha mashauriano hapo jana kabla ya kuanza kwa mkutano wa leo wa kilele.
Duru za jeshi na maafisa wa uwanja wa ndege zimesema Goita aliwasili mjini Accra jana Jumamosi akitokea Bamako.
Goita alihudumu kama makamu wa rais tangu alipoongoza mapinduzi mwezi Agosti mwaka uliopita yaliyomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa kidemokrasia Ibrahim Boubacar Keita.
Nafasi ya rais na waziri mkuu zimekuwa zikishikiliwa na viongozi wa kiraia, Bah Ndaw na Moctar Ouane kufuatia shinikizo kutoka kwa jumuiya ya ECOWAS ambayo imekuwa mpatanishi.