Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Ummy Mwalimu ameigiza Uongozi wa manispaa ya Kinondoni kuhakikisha wanawalipa fidia wananchi waliopisha ujenzi wa Mto ng’ombe kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam( DMDP).
Waziri Ummy amefafanua kuwa wananchi waliohakikiwa na Manispaa ya Kinondoni na kujiridhasha na kiwango stahiki wanachotakiwa kukipata waanze kulipwa kwa kuwa Serikali imetoa Sh 3.5bilioni kwa ajili ya fidia , lakini wanaostahili ni wakazi 375 kati ya 423 baada ya kufanyiwa ukakiki.
Waziri Ummy amesema hayo wakati kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa DMDP awamu ya kwanza katika hicho kilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar esSalaam, Amos Makalla na Mstahiki Meya wa Kinondoni, Mhe. Songoro Mnyonge baada ya hapo alifanya ziara ya ukaguzi wa barabara.
Amesema mchakato umeshafanyika na mtathimin mkuu wa Serikali kila kitu kilikwenda sawa. Hata hivyo kuna changamoto imejitokeza ambapo baadhi ya wananchi wazalendo wametoa taarifa ya kuwa kiwango cha fedha watakachokipata ni kikubwa tofauti na makadirio.
Kwa sasa Manispaa ya Kinondoni inajiridhisha na taarifa hizo na amewataka wakati wakiendelea na mchakato huo waanze kuwalipa wananchi au mwananchi ambaye ameshakikiwa na kiwango anachotakiwa kukipata.
“Msianze kusubiri hadi muhakiki wote hapana mtu ameshahakikiwa na fedha yake sahihi basi alipwe, Tusisubiri hadi wananchi wote, kwa sababu watu wanasubiri hizi fedha kwa muda mrefu kwa ajili ya kufanya maendeleo,” amesema Waziri Ummy.
“Tathmini ya kujiridhisha iendelee lakini wale waliohakikiwa na mkajiridhisha wapewe fedha zao msisubiri haya ndio maelekezo yangu’ alisisitiza”
Awali Mratibu wa kikundi kazi kinachoratibu miradi inayopata fedha kutoka Benki ya Dunia, (TARURA WBWG), Mhandisi Eng. Humphrey Kanyenye alimweleza Waziri Ummy kuwa maandalizi ya mradi wa DMDP awamu ya kwanza yalianza Juni 9 mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kanyenye, utekelezaji wa mradi huo ulianza 2017 na kwamba unatarajiwa kukamilika mwakani.
Amesema jumla ya km 170 za barabara ya Lami kati 206 zimejengwa.