Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemteua Meja mstaafu wa Jeshi, Jessica Alupo kuwa Makamu wa Rais wa Uganda.
Jessica Alupo ambaye amewahi kuwa Waziri wa Elimu wa nchi hiyo anakuwa mwanamke wa pili katika historia ya nchi hiyo kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Museveni pia amemteua Robinah Nabbanja kuwa Waziri Mkuu na kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, kabla ya uteuzi huo Nabbanja alikuwa Naibu Waziri wa Afya.
Kiryowa Kiwanuka, ameteuliwa kuwa mwanasheria mkuu wa Serikali ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa mmoja wa mawakili binafsi wa rais.
Rebecca Kadaga ambaye ni Wakili ameteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa kwanza ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Spika wa Bunge akipewa jukumu la kusimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia, Museveni amefanya uteuzi wa baraza jipya la mawaziri 31 na manaibu waziri 50 huku 10 kati yao wakiwa ni wanawake.
Baraza hilo la Mawaziri pia linajumuisha maafisa wapya kutoka jeshini akiwemo Kamanda Mkuu wa sasa wa majeshi, Jenerali David Muhoozi ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
Aidha, Sam Kuteesa ambaye amekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa muda mrefu ameondolewa katika Baraza la Mawaziri.