Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting umekanusha taarifa za beki wao wa kushoto Edward Charles Manyama ambaye anadaiwa kusaini mkataba wa kuitumikia Simba SC, kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

Manyama amechukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii pamoja na kwenye vyombo vya habari, huku ikiaminiwa ameamua kujilupua katika mpango wa kumtumikia mnyama msimu ujao.

Akizungumza na Dar24Media #taarifabilamipaka Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote, na zinaendelea kuwashangaza wao kama viongozi.

Amesema Manyama hajasaini kwenye klabu yotote mpaka sasa, na tayari ameuthibitishia Uongozi wa Ruvu Shooting suala hilo, kwa njia ya Simu akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’.

“Nimezungumza na Manyama, amenithibitishia kuwa, taarifa hizo ni za uzushi, na amewataka viongozi wengine kuwa watulivu, kwani akimaliza masuala ya timu ya taifa atarejea Ruvu Shooting kuendelea na majukumu yake kama kawaida.”

Hata hivyo Masau Bwire amekiri kuwa, Manyama ajiunga na Ruvu Shooting mwishoni mwa mwaka jana kwa makubaliano ya mkataba wa muda mfupi, lakini akaendelea kusisitiza kuwa, suala hilo haliwezi kuwa sababu ya kukiuka taratibu na mikakati aliojiwekea ndani ya klabu hiyo, yenye maskani yake makuu huko Mlandizi mkoani Pwani.

“Tulipomsajili wakati wa dirisha dogo, Manyama alisaini mkataba wa muda mfupi (Miezi 06), lakini hilo haliwezi kumpa jeuri ya kwenda kunyume na maazimio yake ya kuitumikia Ruvu Shooting, ambayo ilimnasa akitokea Namungo FC.” Amesema Masau Bwire

Hata hivyo mpaka sasa Uongozi wa Simba SC haujasema lolote kuhusu usajili wa beki huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Taifa Stars, kilichoshiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Cameroon.

Manyama aliibukia Biashara United Mara inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, na safari yake ya kuelekea Namungo FC ilichagizwa na aliyekua Kocha wa klabu hiyo Hitimana Thiery, ambaye aliondolewa klabuni hapo mwishoni mwa mwaka 2020, kufuatia mambo kumuendea kombo.

Hitimana alitambua uwezo wa Manyama alipokua Mkuu wa Benchi la Ufundi la Biashara United Mara, kabla ya kutimuliwa na kuibukia Namungo FC mapema msimu uliopita.

Serikali yashauriwa kuanzisha somo la utunzaji mazingira
Manyama asaini miwili Simba SC