Hatimaye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezungumzia msimamo wake kuhusu madai ya Katiba Mpya pamoja na marufuku ya mikutano ya hadhara, akiwataka watanzania kuendelea kuwa na subira.
Rais Samia ameeleza msimamo wake jana alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari katika kuhitimisha siku 100 za utawala wake, Ikulu mkoani Dar es Salaam.
Amesema kuwa hivi sasa amejikita katika kuimarisha uchumi wa nchi kwani umeshuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na athari za ugonjwa wa corona zinazoikabili dunia. Hivyo, amewataka watanzania kuwa na subira kwani baada ya jitihada hizo atashughulikia madai hayo.
“Kama inavyosemwa nimeanza vizuri naomba nipeni muda nisimamishe nchi kwanza kiuchumi. Tuite wawekezaji wawekeze ajira zipatikane uchumi ufunguke halafu tutashughulikia Katiba, tutashughulikia mikutano ya hadhara wakati ukifika,” alisema Rais Samia.
- Rais Samia ataja idadi ya wagonjwa wa corona Tanzania
“Kwa sasa tunaruhusu mikutano ya ndani ya vyama na wabunge wapo huru kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao si maeneo ya wengine…, ile yeyeee ingieni…, hili naomba sana Watanzania tujipe muda tufanye uchumi wetu…, sisemi katiba si ya maana lakini naomba mnipe muda kwanza nisimamishe uchumi kisha tutatizama mengine,” aliongeza.
Aidha, alizungumzia ahadi yake ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa aliyoitoa wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kuwa ataitimiza ahadi hiyo, lakini kwanza anajikita katika kuhuisha uchumi.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefufua harakati za kudai Katiba Mpya, wakiamini ndio mwarubaini wa changamoto kadhaa za kisiasa zinazojitokeza.