Mshambuliaji wa klabu ya AS Vita Club Fiston Kalala Mayele amethibitsha kuwa yupo katika mazungumzo ya kujiunga na klabu ya Young Africans.

Mayele mwenye umri wa miaka 27, amethibitisha taarifa hizo, baada ya taarifa zake na Young Africans kufifia kwa majuma mawili, kufuatia hapo awali jina lake liliwahi kutajwa kwenye mchakato wa watakaosajiliwa Jangwani kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.

Fiston amesema ana ofa nyingi mkononi kutoka klabu za Algeria, Tunisia, Qatar na Saudi Arabia, lakini anavutiwa sana kujiung na Young Africans ya Tanzania.

“Ninatamani kucheza Tanzania, mpaka sasa nimepata ofa nyingi kutoka kwenye nchi kadhaa barani Afrika, lakini Young Africans naipa kipaumbele kwa sababu ninajua nini wanakihitaji kwangu.” Amesema Fiston

Katika msimu wa 2020/21, Mshambuliaji huyo aliifungia AS Vita Club mabao 15, na kuwa mmoja wa wachezaji waliong’ara vizuri kwenye ligi ya DR Congo (Linafoot League).

Tayari Young Africans wanatajwa kukamilisha usajili wa beki wa kulia wa AS Vita Club Djuma Shaban, na huenda akawasili Tanzania wakati wowote baada ya msimu huu 2020/21 kufikia kikomo baadae mwezi huu.

Uongozi wa Young Africans umejipanga kufanya usajili wa wachezaji wenye hadhi ya kushindana wakati wote, ili kufanikisha lengo la kurejesha heshima ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, ambao upo mikononi mwa watani zao wa jadi kwa miaka mitatu mfululizo.

Kamati ya uchaguzi TFF yaitwa Mahakamani
Twiga Stars kambini Julai 03