Fedha zitakazopatikana kwenye tozo ya miamala ya simu na bando za mitandao zitapelekwa kutatua changamoto zililizopo kwenye jamii pamoja na miradi mbalimbali hazitatumika kwa ajili ya kulipa mishahara.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, wakati akizungumza na Chama cha Watoa Huduma wa Simu Tanzania (TAMNOA), ambapo amesema kuwa tozo hizi watanzania wengi wameunga mkono kwa kutambua umuhimu wa maendeleo ambayo kukamilika kwake kunahitaji mchango wao.
“Fedha zitakazo patikana kwenye tozo hizo hazitatumika kulipa mishahara wala kugharamia matumizi mengine yoyote ya Serikali bali zitapelekwa moja kwa moja kutatua changamoto za afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, elimu na mingine mingi ikiwemo miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli ya kisasa na Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere,” amesema Dkt. Nchemba.
“Kampuni za simu msichukulie makato haya kama kodi nyingine mnazowatoza wateja wenu bali Serikali iliamua kuweka makato haya kwenye miamala ya kuweka muda wa maongezi na kufanya miamala kwa njia ya simu ili kuwafanya Watanzania na watumiaji wengine wa simu kuchangia maendeleo ya nchi” amesema Dkt. Nchemba
Aidha, Dkt. Nchemba alitoa muda wa siku 14 kuanzia tarehe 1 hadi 15 Julai, 2021, kwa watoa huduma wote wa Mitandao ya Simu kurekebisha mifumo yao na kuanza kutoza rasmi makato hayo ili Serikali ianze kukusanya fedha hizo.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Simu ya Vodacom Roselynn Mworia, amesema kuwa chama chao kimeupokea mpango huo kwa mikono miwili na kuwataka wateja wao kuiunga mkono Serikali kwa kuendelea kutumia huduma za kupiga simu na kufanya miamala ya simu.