Kiungo Mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia na Cape Town City ya Afrika Kusini, Charles Zulu, amefuzu vipimo na kujiunga rasmi na Azam FC.
Azam FC imefanikiwa kuinasa saini ya kiungo huyo, ikiwa ni maandalizi ya kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu pamoja na Michuano ya Kimataifa.
Imeelezwa kuwa uwepo wa Kocha George Lwandamina, umefanikisha usajili wa kiungo huyo ambaye anatarajiwa kuwa msaada mkubwa huko Chamazi.
Zulu mzaliwa wa Lusaka,Zambia kule wanakotokea Clatous Chota Chama na Rally Bwalya amewahi kuitumikia klabu ya Zanaco ya nchini kwao Zambia kuanzia mwaka 2013-2020 kabla hajajiunga na klabu ya Capetown city ya Afrika ya Kusini.
Ameitumikia timu ya taifa ya Zambia kuanzia ile ya umri wa miaka 17,20,23 na ile ya wakubwa ‘Chipolopolo’.
Katika michezo 14 aliyoitumikia Chipolopolo amefanikiwa kufunga bao moja pekee,bao ambalo alifunga kwenye michuano ya COSAFA 2016 dhidi ya Lesotho ya ushindi wa mabao 3-2.
Azam FC itakuwa sehemu ya timu nne zitakazoiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao, baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika kutangaza mataifa 12 yatakayopeleka timu nne, ikiwemo Tanzania.
Zulu anatarajiwa kutambulishwa na Uongozi wa Azam FC wakati wowote hii leo kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo.