Kocha mkuu wa Klabu Bingwa Barani Afrika Al Ahly ya Misri, Pitso Mosimane amesema mchezo wa klabu bingwa Afrika (CAF Champion League) dhidi ya Simba uliochezwa jijini Dar es salaam na kikosi chake kukubali kufungwa bao 1-0, ulikua mgumu kwake kwa msimu huu 2020/21.
Mosimane ambaye imeifikisha Al Ahly Fainali na itacheza na Kaizer Chiefs July 17 amedai kuwa mchezo huo utabaki kwenye kumbukumbu zake, tangu alipoajiriwa klabuni hapo.
“Mchezo dhidi ya Simba SC utaendelea kubaki kwenye kumbukumbu zangu, ulikuwa mgumu sana kwa wachezaji wangu, walituzidi kila idara na mwisho wa dakika 90 tulipoteza.”
Katika Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, bao Simba SC lilifungwa na kiungo Mshambuliaji kutoka Msumbiji Luis Muquissone.
Katika michezo ya klabu bingwa msimu huu Al Ahly imecheza michezo 12 imeshinda michezo 8, sare 3 na kufungwa 1.
Al Ahly ilitinga Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuiondosha Espirance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-1, Huku Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini wakiing’oa Wydad Casablanca ya Morocco kwa bao 1-0.
Wawili hao watakutana Fainali Julai 17 kwenye Uwanja wa Mfalme Mohammed IV mjini Casablanca, Morocco.