Ni kama Simba SC ametetea taji lakenla VPL kwa mara ya nne mfululizo, baada ya kuibanjua KMC FC katika mchezo wa kiporo wa mzunguuko wa 31 uliochezwa leo Jumatano (Julai 07), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC imemaliza dakika 90 za mchezo huo kwa kupata ushindi wa mabao 2-0, yaliofungwa na Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Criss Mutshimba Koppe Mugalu dakika ya 3 na 44.
Ushindi huo unaifanya Simba SC kufikisha alama 76 ambazo zinaweza kufikiwa na Young Africans pekee, endapo itashinda michezo yake miwili iliosalia.
Kimahesabu ipo hivi: Simba SC ina uwiyano mkubwa wa mabao ya kufunga na kufungwa, na mpaka mchezo dhidi ya KMC FC unamalizika Mabingwa hao wa Tanzania Bara wamefikisha mabao 71 na kufunga huku wakifungwa mabao 13. Hivyo Simba SC ana uwiyano ya mabao ya kufungwa na kufunga 58.
Young Africans wamefunga mabao 50 na kufungwa mabao 21. Hivyo Klabu hii ya Jangwani ina uwiyano wa mabao ya kufunga na kufungwa 29.
Ikitokea Simba SC inapoteza michezo mitatu iliosalia na Young Africans ikishinda michezo yake miwili, Wananchi watatakiwa kufunga zaidi ya mabao 29 ili kumzuia mtani wake kuwa bingwa kwa mara ya nne mfululizo.
Hata hivyo Simba SC ina njia nyingine ya kumaliza mkanganyiko wa kimahesabu kwa kusaka alama moja pekee, katika michezo yake mitatu iliobaki, ili kufikisha alama 77 ambazo hazitaweza kufikiwa na klabu yoyote ilioshiriki Ligi Kuu Msimu huu.
Simba SC imebakiza kucheza dhidi ya Coastal Union, Azam FC na Namungo FC.