Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Pwani kutumia mkakati wa uvunaji wa mifugo kama mkakati wa kumaliza migogoro ya wafugaji na wakulima pamoja na kuondokana na tatizo la uhaba wa malighafi katika viwanda vya kuchakata nyama mkoani humo.

Naibu Waziri Ulega amesema hayo leo (12.07.2021) alipokutana na uongozi wa mkoa huo ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, wakati akitoa taarifa ya ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani na kufafanua kuwa ni vyema uongozi huo ukafanya tathmini ya kina kwa kuunda kamati maalum ili kutafuta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

Amesema viongozi ndani ya mikoa yote nchini ni vyema wakaunda kamati maalum za wataalamu kwenda wilayani hadi vijijini ili kutafuta ufumbuzi wa haraka na kudumu wa kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji, ukiwemo mkakati wa kuhakikisha wafugaji wanavuna mifugo yao kwa kuuza katika viwanda vya kuchakata nyama ili vipate malighafi na kuuza nyama ndani na nje ya nchi.

Mhe. Ulega amesema serikali inalichukulia suala hilo kwa uzito mkubwa kwa kutumia kamati maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Amesema wizara ilishatuma timu ya kushughulikia jambo hilo kwa ngazi ya taifa na imetoka na mapendekezo kadhaa kwa hatua zaidi.

Mhe. Ulega amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasisitiza mikoa kuunda kamati ya wataalam kubaini mambo kadhaa ili kuchukua hatua ili jambo hilo lisijitokeze katika maeneo mbalimbali nchini.

“Timu hizo zitabaini maeneo ya mifugo vamizi, wafugaji wakorofi ili waweze kuchukuliwa hatua kali sambamba na kubainisha mahitaji halisi ya miundombinu ya mifugo, kuwepo kwa taarifa kamili za mifugo ilipo pamoja na kuhamasisha kuwa na utamaduni wa kuuza mifugo kwenye viwanda vya kuchakata nyama ili vipate malighafi.” amesema Mhe. Ulega.

Akizungumzia hali halisi ya hatua zilizochukuliwa na Mkoa wa Pwani kukabiliana na kero hiyo mkuu wa mkoa huo Mhe. Abubakar Kunenge amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutochukua sheria mkononi na kuviasa vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki wanapopata taarifa ya migogoro hiyo.

Mhe. Kunenge amefafanua kuwa mkoa huo tayari umeanza kufanya sensa ya mifugo katika wilaya zote na Wilaya ya Rufiji kwa sasa ipo hatua za mwisho kukabidhi mapendekezo yao.

Ameongeza kuwa taarifa hiyo ya sensa wamebaini kuna wafugaji wengi waliopo katika wilaya hiyo hawajasajiliwa na hawana taarifa zozote za wanakotoka wala wanakokwenda.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa katika Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani ameagiza uongozi huo pamoja na wizara wanaohusika na masuala ya chanjo kuhakikisha chanjo zinazozalishwa na taasisi hiyo zinawafikia wafugaji waliopo vijijini badala ya kuanza kufikiria kusambaza chanjo hizo nje ya nchi.

Mhe. Ulega amesema kuna mifugo mingi kama kuku, ng’ombe na mbuzi wanaokufa kwa kuwa wafugaji hawajui kama kuna chanjo zinazozalishwa hapa nchini ingawa kuna maeneo mengine chanjo hizo hazijafika kabisa.

Ametaka viongozi hao kuhakikisha chanjo zinafika maeneo mbalimbali nchini hususan maeneo ya vijijini ili wafugaji waweze kukinga mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali.

Mhe. Ulega ametembelea pia kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER kilichopo Wilayani Kibaha na kujionea namna kiwanda hicho kikiwa tayari kuanza kuzalisha chanjo ambazo zitakuwa zikiuzwa ndani na nje ya nchi.

Akiwa kiwandani hapo ameendelea kusisitiza chanjo za mifugo kufikishwa maeneo mbalimbali nchini hususan ya vijijini ili mifugo iwe na afya bora na wafugaji waweze kunufaika kupitia ufugaji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akizungumza mara baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kuanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo ambapo ameusisitiza uongozi wa mkoa huo kuwa na mkakati wa kumaliza migororo ya wakulima na wafugaji ikiwemo njia ya kuhamasisha wafugaji kuvuna mifugo yao na kuuza viwandani ili viwanda hivyo vipate malighafi kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya nchi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge akibainisha mikakati ya mkoa katika kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji wakati Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega alipofika ofisini kwake kabla ya kuanza rasmi ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo, ambapo Mhe. Kunenge amewataka wakazi wa mkoa huo kutochukua sheria mkononi na kuvielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki vinapopata taarifa juu ya migogoro hiyo. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akioneshwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi, sehemu ya eneo la Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani ambalo limevamiwa na baadhi ya wananchi na kujenga makazi. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, (wa tatu kutoka kushoto) akioneshwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dkt. Stella Bitanyi moja ya mitambo inayotumiwa na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya Kibaha, Mkoani Pwani. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akiangalia moja ya mitambo katika kiwanda cha kuzalisha chanjo za mifugo cha HESTER kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na kusisitiza chanjo zinazozalishwa nchini zinapaswa kufikishwa maeneo ya vijijini ili wafugaji wakinge mifugo yao dhidi ya magonjwa mbalimbali. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Maoni ya wananchi yasidharauliwe - Warioba
Mhandisi Kundo atoa maelekezo kwa watoa huduma kuhusu ulinzi wa minara ya mawasiliano