Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amezungumzia kuhusu umuhimu wa Katiba mpya, na kutaka maoni ya wananchi yasipuuzwe kwa kuwa ndiyo mara yao ya kwanza kushirikishwa kuitengeneza.

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 ITV amesema kuwa ni muhimu mchakato wa Katiba mpya ukakamilishwa kwa kufikiria hatua ya kuchukua kuanzia ilipoishia mwaka 2014.

Jaji Warioba amesema kuwa  Katiba ni muhimu na imefika hatua kubwa ya kuwa na katiba mpya, kwani sheria na Tume iliundwa ili kupata maoni ya wananchi na ilizunguka nchi nzima kuyakusanya, na mambo yaliyokuwapo katika Rasimu ya Tume yalichukuliwa Bunge Maalum la Katiba yalitokana na maoni ya wananchi.

“Usije ukasema Katiba siyo muhimu wakati wananchi wanasema ni muhimu, tulipofikia ni hatua muhimu tunachotakiwa ni kutafakari kwamba tunamaliza vipi na lini, hata nilipomsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan, hakusema kwamba tusimalizie hiyo, anazungumzia lini.” amesema Warioba

Jaji Warioba ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, amesema katiba za zamani walikuwa hawaulizwi wananchi, na kwamba kwa mara ya kwanza mwaka 2014 iliyoandaliwa ilipata maoni ya wananchi, hivyo maoni ya wananchi yasidharauliwe.

Serikali yakutana na taasisi, mashirika na mabalozi kujadili mapato na matumizi ya bajeti
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ataka kumalizika kwa migogoro na chanjo kufikishwa vijijini