Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ameusisitiza uongozi wa Mkoa wa Pwani pamoja na Wizara inayohusika na maswala ya Chanjo kuhakikisha chanjo zinzozalishwa na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) zinawafikia wafugaji waliopo vijijini badala ya kuanza kufikiria kusambaza chanjo hizo nje ya nchi.
Amesema hayo alipokutana na uongozi wa mkoa huo ambapo amewataka viongozi ndani ya mikoa yote nchini ni vyema wakaunda kamati maalum za wataalamu kwenda wilayani hadi vijijini ili kutafuta ufumbuzi wa haraka na kudumu wa kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji,
Ulega amesema wizara ilishatuma timu ya kushughulikia jambo hilo kwa ngazi ya taifa na imetoka na mapendekezo kadhaa kwa hatua zaidi.
Aidha amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi inasisitiza mikoa kuunda kamati ya wataalam kubaini mambo kadhaa ili kuchukua hatua ili jambo hilo lisijitokeze katika maeneo mbalimbali nchini.
“Timu hizo zitabaini maeneo ya mifugo vamizi, wafugaji wakorofi ili waweze kuchukuliwa hatua kali sambamba na kubainisha mahitaji halisi ya miundombinu ya mifugo, kuwepo kwa taarifa kamili za mifugo ilipo pamoja na kuhamasisha kuwa na utamaduni wa kuuza mifugo kwenye viwanda vya kuchakata nyama ili vipate malighafi.” amesema Ulega.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amewataka wakazi wa Mkoa wa Pwani kutochukua sheria mkononi na kuviasa vyombo vya ulinzi na usalama kutenda haki wanapopata taarifa ya migogoro hiyo.
Kunenge amefafanua kuwa mkoa huo tayari umeanza kufanya sensa ya mifugo katika wilaya zote na Wilaya ya Rufiji kwa sasa ipo hatua za mwisho kukabidhi mapendekezo yao, ambapo ameeleza kuwa taarifa hiyo ya sensa imebaini kuna wafugaji wengi waliopo katika wilaya hiyo hawajasajiliwa na hawana taarifa zozote za wanakotoka wala wanakokwenda.