Klabu ya AS Vita ya mjini Kinshasa, DR Congo inaendelea kubomoka kwa kuondokewa na wachezaji muhimu wakitanguliwa na Kocha Florent Ibenge.
Imefahamika kuwa beki wa klabu hiyo iliyopokwa ubingwa wa DR Congo msimu wa 2020/21 kwa makosa ya usajili, Vivien Assie (Kushoto) amethibitisha kuvunja mkataba wake klabuni hapo.
Beki huyo raia wa Ivory Coast mwenye umri wa miaka 28 amesema ameamua kuvunja mkataba na AS Vita Club ili apumzike nyumbani na familia yake.
Vivien aliyejiunga na As Vita Club Agosti 2020 kwa mkataba wa miaka miwili, amedai kuwa akiwa klabuni hapo alipata majeraha mfululizo, jambo ambalo lilimtokea kwa mara ya kwanza kwenye historia ya maisha yake ya soka.
Hata hivyo beki huyo ameondoka Kinshasa kwa wema, baada ya kumshuku Rais wa AS Vita Bestine Kazadi na mashabiki wa klabu hiyo.
Tayari AS Vita Club imeshampoteza beki wa kulia Djuma Shaaban anayedaiwa kujiunga na Young Africans huku Mshamabuliaji Fiston Mayele akitajwa kuwa kwenye mpango wa kuihama klabu hiyo katika kipindi hiki.
Young African inadaiwa kuwa sehemu ya klabu zinazohitaji huduma ya Mshambuliaji huyo, kufuatia kupendekezwa na Kocha Nabi.