Hali si shwari ndani ya klabu ya Simba SC kufuatia kauli tata zinazoendelea kutolewa na Mkuu wa Idara ya Habari ya klabu hiyo Haji Sunday Ramadhan Manara.
Jana Jumatano (Julai 21) Manara alianza kama utani katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa kuandika mambo ambayo yalichukuliwa kama maskhara, huku akisema ataacha kazi baada ya mpambano wa Fainali Kombe la Shirikisho utakaopigwa Kigoma dhidi ya Young Africans Jumapili (Julai 25).
Hali imeendelea kubadilika kwa Manara hadi kufikia hatua ya kutaja anayofanyiwa ndani ya klabu ya Simba SC kwa kumuanika hadharani Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez kwa kudai amekua na chuki dhidi yake.
Andiko la Manara dhidi ya kiongozi huyo limejikita katika madai ya tuhuma anazorushiwa kwa kudaiwa kwenda Kigamboni kwenye Kambi ya Young Africans kwa lengo la kuihujumu Simba SC.
Manara ameandika: “Barbara una chuki kubwa kwangu, hadi naogopa kula chakula mbele yako. Naacha hii timu kwa ajili yako kwa sababu ya chuki yako kwangu. Unajiona wewe ni Simba kuliko wote, unataka umaarufu kinguvu”
“Nasingiziwa eti nilienda Kigamboni kwenye kambi ya Yanga, vitu hivi ni vya hovyo kabisa. Mimi sinunuliki kwa thamani ya fedha, Barbara kwangu haya ni matusi”
“Barbara amekuwa akinitishia kunifukuza kazi, na kusema Simba sc ni yako na ya Mo. Nimefanya kazi muda mrefu bila mkataba kwa kulipwa mshahara wa laki saba”
“Nimetengeneza imani kubwa kwa mashabiki wa Simba, namuhakikishia Barbara atakuwa wa kwanza kuondoka Simba kabla yangu”
“Unadharirisha wafanyakazi, kwa nini, Dkt. Kashembe umemfukuza kazi,unashida gani ? Shida yako umaarufu ? Unenitumikisha kwa muda gani bila kunilipa ? Mimi niende Kigamboni niihujumu Simba ? Haiwezekani hata kwa pesa yoyote ile”
“Unatamba wewe ndio mwenye timu na Mo, sawa. Tutawaambia mashabiki na naituma hii crip mashabiki wajue. We unaijua Simba ! toka wapi wewe ? Nimewekeza jasho langu hapa Simba miaka mingi lakini leo hii useme nilikuwa Kigamboni! Lini nimeenda Kigamboni mimi ?!
Haji Manara msemaji wa Simba SC