Mwenyekiti wa klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Murtaza Mangungu, amewaomba Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo kuelekeza akili zao kwenye mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho dhidi ya Young Africans utakaochezwa kesho Jumapili (Julai 25), Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Mangungu ametoa rai hiyo kwa Mashabiki na Wanachama, kufuatia sakata la Afisa Habari wa klabu hiyo Haji Manara dhidi ya Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez, ambalo liliibuka Jumatano (Julai 21) kwenye mitandao ya kijamii.
Kiongozi huyo amesema hakuna haja kwa Wanachama na Mashabiki kulipa uzito sakata hilo na kusahau jukumu lao la kuipa nguvu timu kuelekea mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho.
Amesema suala la wawili hao litajadiliwa kwenye vikao vya ndani vya uongozi kwa sababu wote ni waajiriwa wa Simba SC, hivyo kwa muda huu ni vyema mawazo na akili vikaelekezwa mkoani Kigoma.
“Wote wanaolumbana ni waajiriwa na muajiri yupo baada ya mashindano, tathmini ya MWENENDO mzima wa timu na watendaji wake itafanyika…
“Kwa sasa kila mmoja wetu azingatie nidhamu, hekima na MISINGI ya ajira au nafasi yake katika klabu.
Lakini Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Manara ameahidi Jumatatu (Julai 26) ataendeleza sakata lake dhidi ya Barbara.