Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ametengua uteuzi wa Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wa Mkoa wa Kagera Irene Shayo kuanzia tarehe 30/07/2021 kwa kile kilichobainika kuwa taratibu za uteuzi wake zilikiukwa na utumishi wake umekuwa wa kusuasua.
Aidha Shayo amekuwa mtu wa kukwepa sana ziara za viongozi katika eneo lake pamoja na kupika taarifa za mapato na matumizi.
Mhandisi Kundo ameyazungumza hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Kagera ambapo ametembelea ofisi za TTCL na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na kuona kuwa Meneja wa TTCL katika Mkoa wa Kagera hatoshi kuwa katika nafasi hiyo.
“Ninaagiza Meneja wa Mkoa wa Kagera aondoshwe mara moja katika Mkoa wa Kagera na kuanzia leo asitambulike kama Meneja wa Mkoa wa Kagera, taratibu zifuatwe na apangiwe kazi zingine kulingana na wasifu wake kitaaluma ili aweze kufanya kazi vizuri kwasababu majukumu ya sasa hana uwezo nayo”, Amesema Mhandisi Kundo.
Naibu Waziri Muhandisi Kundo amesema kuwa kama Wizara kupitia kwa Waziri mwenye dhamana Dkt. Faustine Ndugulile wana kasi ya kutaka kuona matokeo ya kile ambacho Serikali imedhamiria kukifanya kwa watanzania katika Sekta ya Mawasiliano
Amesisitiza ili kufanikisha hilo ni wajibu wao kufanya maamuzi ya kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zinaimarisha mifumo ya utendaji kazi katika ngazi za mikoa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya watanzania.
Naibu Waziri Mhandisi Kundo, yupo katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kukagua miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ambapo ametembelea katika wilaya ya Muleba, Bukoba na Misenyi na amepanga kuendelea katika Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Ngara.
Ziara yake katika Mkoa huo imeanza tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2021.