Aliyekuwa Afisa Habari wa klabu ya Simba SC Haji Sunday Manara amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kuachana na klabu hiyo mwishoni mwa mwezi Julai.
Manara aliondolewa kwenye nafasi yake Simba SC, kufuatia purukushani zilizoibuka kati yake na Afisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez siku chache kabla ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho ASFC.
Manara amezungumza na wanahabari leo mchana na kueleza kinaga ubaga maisha yake ndani ya klabu ya Simba SC, huku akiainisha baadhi ya madhira anayodai kufanyiwa na viongozi wa juu.
Manara amesema: “Vitu vilivyoniondoa Simba, moja ni Biashara na la pili ni Umaarufu. Sijui lini niliwahi kutamka mimi ni Mkubwa kuliko Simba. Wakati naanza kazi Simba niliambiwa nijitolee malipo yangefata baadae. Nilikubali huku nikijua aliyeniomba yeye alikuwa analipwa.”
“Sijawahi kugombana na mwandishi yeyote kwa sababu ya masuala yangu binafsi, yote hii ilikuwa ni kwasababu ya Simba Sc, ni katika kutetea kiongozi au mchezaji pamoja na brand ya Simba, mimi sio mkamilifu katika kufanya kazi lazima kuna kukosea”
“Nawashukuru sana Yanga Sc wenyewe wanajiita Dar Es Salaam Young Africans hasa katika kipindi hiki cha usajili, yawezekana utani ulizidi ila lengo langu lilikuwa ni kudumisha utani wa jadi, pale nilipokosea wanisamehe na najua niliwakosea”
“Wanasema hakuna mtu mkubwa kuliko Simba Sc, hapana hiyo ni haramu, kwani kuna mahali niliwahi kusema Haji ni Mkubwa? nimefanya makubwa sana katika kuhamasisha timu, mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni”
“Mkiniona mikoani mjue najitegemea, Msemaji anayepiga promo kubwa na anaisemea timu, nauli anajitegemea, kula anajitegemea, hoteli anajitegemea hadi safari za nje anajitegemea, kila wakisafiri naambiwa jina lako halipo”
“Simba walikuwa wanatoa bonasi za mechi lakini sijawahi kupata hata senti moja, promo zote nafanya lakini sikupewa chochote, hata hela ya mafuta tu ya kwenda kufanyia promo kwenye redio sipewi, juzi tu ndo wamenipa laki mbili tena kwa mbinde”
“Senzo alipokuja walimwambia anifukuze mimi hata bila sababu, akakataa akasema namfukuza vipi wakati sijafanya nae kazi, sijui utendaji kazi wake, mabosi wakaacha kuchukia hata yeye alishindwa kuvumilia kutokana na kuingiliwa majukumu yake akapata ofa nono akaondoka”
“Mkataba wa milioni tatu walionipa ulikuwa na sharti la kutangaza bidhaa za Mo, nikakataa nikawaambia ivi mnanijua au mnanisikia, baadae wakamwambia Barbara arekebishe, wakaja wakasema siruhusiwi kutangaza kampuni inayoshindana kibiashara na kampuni zinazoidhamini Simba ambazo zipo Azam”
“Nilikataa kitu Kama hicho baadae MO akaanza kubadilika kwamba waanze kunitoa Simba, kuna siku Mo alinipigia simu akasema watu wanasema umeanza kuwa maarufu kuliko Mimi inabidi tukutoe, nikasema sawa”.