Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla ameagiza kusimamishwa kwa ukusanyaji wa Michango yote ya Elimu mashuleni baada ya michango hiyo kugeuka kero na mzigo kwa walezi na wazazi wa wanafunzi kinyume na mwongozo wa waraka wa Elimu Bure.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea kero za Wananchi kwenye Mwendelezo wa ziara yake ya kusikiliza Migogoro Jimbo la Segerea ambao Wazazi wamedai wamekuwa wakichangia kiasi Cha Shilingi 300 hadi Tsh 1,000 kwaajili ya gharama za uchapaji wa mitihani kinyume na waraka wa Elimu bure.
Kutokana na hilo RC Makalla ametaka utaratibu wa michango utokane na maazimio ya kikao Cha Wazazi wa shule husika kukubali na kibali kifike ofisi yake ajiridhishe ndipo atoe ruhusa.
Aidha RC Makalla pia ametaka michango ya miradi ya maendeleo mashuleni itokane na maazimio ya kikao Cha Wananchi na sio watu wachache kujiamulia na kuamuru Wananchi kuchanga kwa lazima.