Serikali ya Canada imeahidi kuisaidia Tanzania kuimarisha Sekta ya Afya, Elimu na Mazingira kutokana na ufanisi katika usimamizi wa fedha na miradi inayotekelezwa nchini kwa ushirikiano wa Serikali hiyo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Jijini Dodoma wakati wa mkutano wake na Balozi wa Canada Nchini Tanzania, Pamela O’Donnell, ulioangazia ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Amesema kuwa Tanzania na Canada zitaanzisha mazungumzo mapya ya namna ya kuendeleza programu za maendeleo zilizokuwa zikifadhiliwa na Serikali ya Canada baada ya progamu iliyokuwepo kumaliza muda wake mwezi Juni, 2021.

Aidha nchi ya Canada imeisaidia Tanzania katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Sekta ya madini, elimu, afya na utawala bora yenye thamani ya takribani dola bilioni 2.39 tangu Tanzania ilipopata uhuru.

Kwa upande wake Balozi wa Canada Nchini Tanzania, Pamela O’Donnell, amesema kuwa kuna mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika miradi mbalimbali iliyotekelezwa nchini Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada hususani katika Mfuko wa Afya na Elimu, ambapo fedha zilizotolewa zimetumika kikamilifu katika masuala yaliyokusudiwa.

“Kutokana na jitihada za Serikali katika kutekeleza miradi, tunaona kuna fursa ya kuendeleza ushirikiano katika masuala mbalimbali ikiwemo elimu, afya na kuwajengea uwezo wanawake”, Amesema Balozi Pamela O’Donnell.

RC Makalla apiga 'stop' michango holela mashuleni
Video: Kesi ya Mbowe na wenzake kuunguruma tena Septemba 3