Askari 72 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwenye vituo mbalimbali vya Viwanja vya Ndege nchini wamepandishwa vyeo vya ukoplo baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya uongozi yaliyofanyika kwenye Chuo cha Jeshi hilo cha Chogo kilichopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga.

Akiwatunuku vyeo hivyo leo septemba 1, wazimamoto wa kiwanja Cha Ndege Cha Kimataifa Cha Julius Nyerere JNIA, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi hilo, ambaye pia ni Mkuu wa Zimamoto na Uokoaji kwenye Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA), SACF Elia Kakwembe amewataka wahitimu hao kuendelea kufanya vyema kwa kujituma zaidi kwenye majukumu yao na sio kubweteka baada ya kupewa cheo hicho. maana bado wapo chini ya uangalizi.

Wazimamoto waliotunukiwa vyeo hivyo ni kutoka Viwanja vya ndege vya Mwanza, Dodoma, Lindi, Mpanda, Kigoma, Kilwa Masoko, Moshi, Arusha, Manyara, Mtwara, Masasi, Musoma, Shinyanga, Songea, Tabora, Tanga, Songwe na Julius Nyerere JNIA).

Hata hivyo, wazimamoto hao ni miongoni mwa Wazimamoto 400 wa jeshi hilo waliopata mafunzo  hayo kwa nchi nzima, ambapo wengine wapo kwenye vituo vingine tofauti na viwanja vya ndege.

“Sasa msiende kutambia baa hivi vyeo mjue cheo ni dhamana, tunataka muendelee kufanya vizuri maana nyie mmeshakuwa viongozi na mtakuwa mnafuatiliwa kwani cheo sio kabila wala jina la mtu na ukifanya ndivyo sivyo kinaondolewa mara moja na tutaendelea kuwafuatilia,” Amesema Afande Kakwembe.

Aidha amewataka Wazimamoto hao kuwa wabunifu kwa kuibua mambo mazuri ya kuifanya JNIA kusonga mbele zaidi katika masuala ya uzimajimoto na uokoaji.

Naye Kaimu Kamanda wa Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha JNIA, Mkaguzi Maria Luoga amewataka wahitimu hao kuzingatia Uzalendo wa nchi.

Waliosababisha madhara ya chanjo kwa mifugo kukiona
Mfaume Mfaume ampinga Mwakinyo