Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amemkingia kifua Mshambuliaji wake kutoka DR Congo Chriss Mugalu, kufuatia kuzongwa na wadau wa soka nchini, kutokana na kushindwa kuonesha kiwango chake halisi kwenye mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Young Africans Jumamosi (Septemba 25), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Gomes amesema bado anaimni na Mshambuliaji huyo, na kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Young Africans amekipokea kama changamoto ambayo hutokea kwa wachezaji wote duniani kushindwa kufunga wanapopata nafasi.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa amewahimiza Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kuwa na subra, na wasiendeshwe na mihemko ya mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mshambuliaji wao Mugalu.
“Ni Jambo la wakati tu, kwa mchezaji kama Mugalu kuwathibitishia bado ana kiwango kikubwa cha kucheza na kufunga mabao kama zamani, haina haja kwa Mashabiki wa Simba kuendeshwa na mihemko inayozalishwa kwenye mitandao ya kijamii,”
“Kilichotokea kwenye mchezo dhidi ya Yanga ni kawaida kwa wachezaji wote duniani, hutokea mara kwa mara, kwangu kama kocha nimelipokea hilo kama changamoto, na tayari nimeshazungumza na Mugalu.” amesema Kocha Gomes
Katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22 dhidi ya Biashara United Mara, Chriss Mugalu hakupata nafasi ya kucheza na badala yake kocha Gomes aliwatumia John Bocco na Meddie Kagere.