Maofisa wa ngazi za juu wa Ulinzi wa Marekani wamesema hatua ya Taliban kurejea madarakani nchini Afghanistan imetokana na mkataba kati ya kundi hilo na utawala wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump.
Mkataba huo unaojulikana kama makubaliano ya Doha ulisainiwa Februari 2020 na kuweka tarehe ya kuondoka kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani kwenye ardhi ya Afghanistan.
Mbali na kuweka tarehe ya mwisho ya vikosi vya Marekani kuondoka Afghanistan, makubaliano ya Doha yalijumuisha pia majukumu mapana kwa Taliban kuchukua hatua za kuzuia makundi kama vile al-Qaeda kutishia usalama wa Marekani na washirika wake.
Jenerali Frank McKenzie amesema makubaliano hayo yalikuwa na athari mbaya kwa serikali ya Afghanistan na Jeshi lake na Kauli hiyo imeungwa mkono na Waziri wa ulinzi Lloyd Austin anayesema makubaliano hayo yaliisaidia kikundi cha Taliban kujiimarisha zaidi.
Baada ya kuchaguliwa kwake, Rais wa Marekani Joe Biden aliendeleza mpango huo wa Marekani kujiondoa lakini kwa kuongeza muda mpaka Agosti 31, badala ya mwezi Mei.
Jenerali McKenzie alisimamia zoezi la kuondoka kwa vikosi vya jeshi la Marekani nchini Afghanistan, lililohitimisha miaka 20 ya uwepo wake nchini humo ikiwa ni vita vya muda mrefu zaidi katika historia ya Marekani.
Maafisa hao wa ulinzi wa Marekani wameyasema hayo Jumatano hii mbele ya Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo.