Serkali imefuta leseni ndogo 175 za wachimbaji mkoani Kagera ambazo wamiliki wake wanadaiwa tozo za Serikali na zilizokwisha muda wake.
Leseni hizo zimefutwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiwa katika Mgodi wa Sindiketi unaochimba madini ya bati uliopo Kata ya Nyaruzumbura wilayani Kyerwa.
Ametoa agizo hilo baada ya mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate kuomba wachimbaji wadogo katika mgodi huo wapewe maeneo ya kuchimba ili waweze kujiongezea kipato na kuchangia mapato ya Serikali.
“Hao wanaodaiwa tuliwapa siku 90 wakashindwa kulipa, naagiza wanyang’anywe leseni zao na waongezewe muda wa kulipa madeni,” alisema Biteko.
Wakati huohuo, Waziri Biteko amemtaka Meneja wa Madini Mkoa wa Kagera, Lukas Mlekwa kusimamia utoaji wa mikataba kwa wachimbaji wadogo kutoka kwa wenye leseni ambayo haitawafunga kuuza madini yao kwenye soko wakishalipa asilimia 20 ya wenye leseni.
“Nasema hivyo kwa sababu hawa watu wanapata shida, mikataba waliyonayo sasa na wenye leseni inawafunga, wanalazimika kuuza madini kwa mwenye leseni. Sasa hii basi, simamia hili,” amesema Biteko.
Awali, Mlekwa alisema leseni 55 ambazo wamiliki wake wameshapewa hati, zinadaiwa Sh1.1 bilioni.
Mlekwa alisema kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Julai hadi Septemba, ofisi ya madini imekusanya Sh1 bilioni huku madini ya bati yakichangia Sh99.1 milioni sawa na asilimia 132 hivyo kuvuka lengo.