Mshambuliaji kutoka nchini Serbia na klabu ya Fiorentina ya Italia, Dusan Vlahovic ameonesha kuwa na ndoto ya kutaka kuitumikia klabu ya Juventus.

Ndoto za Mshambuliaji huyu kuitaka Juventus, zimeanikwa hadharani kwenye gazeti la michezo la kila siku nchini Italia liitwalo ‘Gazzetta dello Sport’.

Kwa mujibu wa ripoti iliyoandikwa kwenye gazeti hilo, Vlahovic ndoto yake kubwa ni kujiunga na miamba ya soka la Italia, mara tu, mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu ujao.

Majaliwa ya Vlahovic yalianza kuwa kwenye shaka huko Fiorentina baada ya msimu uliopita kunukuliwa akisema anataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, Fiorentina wenyewe bado wana matumaini makubwa ya kumbakiza fowadi huyo ambaye yupo kwenye kiwango bora zaidi kwa sasa.

Mkataba wa sasa wa nyota huyo na Fiorentina utamalizika mwaka 2023 na Vlahovic mwenyewe yupo radhi kuondoka hata mwezi Januari mwakani.

Licha ya yeye mwenyewe kuitaka zaidi Juventus, lakini Manchester City, Tottenham Spurs, Atletico Madrid, Inter Milan na Arsenal pia zimekuwa zikiwania huduma ya Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21.

Wachimbaji 175 wafutiwa leseni
Sekta ya Posta ni muhimu - Dkt. Yonazi