Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi ameizungumzia Sekta ya Posta kuwa ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchina dunia kwa ujumla kwasababu inawezesha usafirishaji wa mizigo popote duniani.

Amesema hayo wakati akifungua semina ya watoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na vifurushi nchini wenye leseni ya kufanya huduma hizo kutoka Mamlaka ya Mawasilian Tanzania (TCRA) kwa lengo kujadili maendeleo na maboresho ya Sekta hiyo nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Shirika la Posta Tanzania na wadau wake wanaadhimisha wiki ya Posta duniani ambayo kilele chake ni tarehe 9/10/2021.

Amesema kuwa Serikali imewekeza katika Sekta ya Posta ili kuhakikisha kunakuwa miundombinu rafiki ya usafirishaji na ugavi huku akiitaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na mfumo wa anwani za makazi na Posti kodi ambazo hadi sasa halmashauri 21 nchini tayari zimeshafikiwa na mipango inaendelea kwa nchi nzima kufikiwa na
muundombinu huo

Ameongeza kuwa mfumo huo unaohusisha majina ya mitaa, barabara na namba za nyumba itawezesha na kurahisisha uchukuaji na ufikishaji wa mizigo pamoja na ufikishaji wa huduma mbalimbali kama zimamoto na polisi pale zinapohitajika.

Aidha, amesema kuwa kwa upande wa postikodi kila kata sasa ina postikodi yake na zinatambulika katika mfumo wa postikodi na mwananchi anaweza kufahamu postikodi yake kwa kupiga 15200# na kufuata maelekezo ambayo yatampatia namba ya postikodi ya eneo husika na kwa sababu namba hizi zinatofautiana zinarahisisha mhusika kufikiwa pale alipo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabir Kuwe amesema Mamlaka hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na watoa huduma wa Sekta ya Posta angalau mara mbili kwa mwaka kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu Sekta hiyo nchini na kipindi hiki kinawaunganisha pamoja kuelekea maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia TCRA imeruhusu ushindani katika Sekta ya Posta ili kuboresha utoaji wa huduma, ubunifu na kuleta tija kwa taifa katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa kuyapatia leseni makampuni binafsi yanayofanya huduma za usafirishaji

Naye Afisa Masoko wa DHL, Abdallah Sharrif amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yametoa fursa kubwa kwao kama watoa huduma ya usafirishaji kujumuika na Shirika la Posta Tanzania pamoja na mashirika mengine ya usafirishaji na mawasiliano nchini.

Dusan Vlahovic anavyoiota Juventus
Czech kuwekeza Tanzania