Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema jumla ya Shilingi milioni 107 zimepatikana kwa ajili ya kununua mbegu Bora za kilimo ili kuwasaidia Wakulima ambao mashamba yao yaliharibiwa na mafuriko ya Mto Rufiji Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Meja Gowele ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kupokea msaada wa magodoro 50 na mifuko 150 ya unga wa uzito kilo 10 kutoka huduma ya Arise and shine inayoongozwa na Boniface Mwamposa aliyewakilishwa na Mchungaji Emmanuel Sanga.

Amesema Waziri na Mbunge wa jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa ametoa shillingi milioni 50, wakazi wa Rufiji wanaoishi nje ya Wilaya hiyo wametoa shilingi milioni 13. 7 na Wakuu wa mikoa 26 shilingi milioni 44 na kufikia kiasi hiko cha shilingi milioni 107. 7.

“Tumeshaanza kufanya mchakato kupitia Maafisa Kilimo wanaohusika kwa ajili ya kufanya manunuzi ya mbegu ilitupate mbegu zitakazowatosheleza wakulima wetu, Wizara ya kilimo imeshafanya tathimini ya kupata mbegu kwa ajili ya kuwasaidia Wananchi pindi maji yatakapopungua ili waendelee na shughuli zao za kilimo,” alisema Meja Gowele.

Akizungumzia ugawaji wa viwanja vya makazi mapya ya Waathirika hao katika eneo la Kata ya Chumbi na Muhoro Meje Gowele alisema Wakala wa misitu Tanzania –  TFS, Wilaya ya Rufiji imetoka maeneo ya viwanja 600, ili Wananchi hao wapate makazi na mabonde wayatumie kwa Kilimo pekee.

Polisi wazindua elimu ya usalama Barabarani kwa Wanafunzi
Dkt. Ndumbaro asisitiza matumizi sahihi maeneo ya wazi