Mawakili wanaotoa msaada wa kisheria kwa watuhumiwa wa makosa mbalimbali yakiwamo ya jinai, wameshauriwa kutekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao na si vinginevyo.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Tanganyika ( TLS) muda mfupi baada ya Ujumbe wa Makatibu Wakuu kumaliza mazungumzo yao na mahabusu na wafungwa wanaume na wanawake waliopo katika Gereza la Bukoba.
Ushauri huo umetokana na kisa cha mahabusu mmoja ambaye amekaa ndani ya gereza hilo kwa zaidi ya miaka sita akisubiri kukamilika kwa upepelezi wa tuhuma za mauaji anazokabiliwa nazo.
Mahabusu huyo aliwaeleza Makatibu Wakuu hao, kwamba licha ya yeye kuwa tayari kukiri kosa lake na alikuwa tayari kufanya hivyo, lakini Wakili aliyekuwa anamsimamia alimkataza kukiri kosa lake kitendo ambacho kimemfanya aendelee kusota Gerezani.
“ Hapana naona kuna shida ya maadili hapa hakuna jambo jingine Bw. TLS, nikuombe hebu kaa na mawakili wako muliangalie hili, Kama mtuhumiwa anataka mwenyewe kwa hiari yake kukiri kosa lake mwacheni afanye hivyo, kwa sababu yeye ndiye anayejua ukweli wa nini alichokifanya, shaurini vizuri zingatieni maadili ya kazi zenu na taaluma zenu”. Akasisitiza Katibu Mkuu Mchome.
Katibu Mkuu Mchome, ameongeza kuwa kazi kubwa ya Mawakili na Wanasheria ni kutoa ushauri wa kisheria kwa weledi, maadili mema, kwa wakati na kufanya kazi kwa matokeo ili haki itendeke na taifa liendelee kupiga hatua za maendeleo.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Profesa Mchome amesema, atatuma timu ya Wanasheria Kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ili kwenda kutoa msaada wa kisheria Mkoani Kagera.