Rapa Jay Z amerejea kujiunga na familia ya watumiaji wa mtandao wa Instagram Duniani ambapo ndani ya masaa matatu pekee tangu kujiunga kwake, Jay z amefanikiwa kupata wafuasi (followers) zaidi ya Milioni moja.
Hov kupitia akaunti yake hiyo amemfuata mtu mmoja pekee ambaye ni mke wake mwanamuziki maarufu Duniani Beyoncé Giselle Knowles-Carter.
Kujiunga kwa Jay Z kwenye mtandao huo kunajibu maswali ya mashabiki wa rapa huyo ambao wengi walikuwa wakihoji ni ipi sababu ya yeye kuamua kuupotezea kwa miaka mingi mtandao huo, licha ya kundi kubwa la wasanii na wajasiriamali Ulimwenguni kuwa limejikita katika matumizi ya mitandao ya kijamii hasa instagram ikiwa ni sehemu muhimu ya kukuza biashara kwa kukutana na matabaka mbali mbali ya wateja.
Inaweza kuwa Jay Z alikuwa akiichukia sana mitandao ya kijamii.
Hili linakuja kufuatia maneno aliyowahi kuyazungumza rapa Meek Mill kuhusu alichowahi kuambiwa na Jay Z.
Licha ya kuitumia lakini rapa Meek Mill pia amewahi kuwa mmoja wa watu wenye kuichukia sana mitandao ya kijamii, na aliwahi kueleza masikitiko yake kupitia chapisho kwenye mtandao wake wa Instagram, ambapo katikati ya alichokiandika aliweka maneno ya busara ya Jay Z, yakifichua kile ambacho alikuwa akifikiria kuhusu mitandao ya kijamii.
“Jay Z aliwahi kuniambia kuwa ulimwengu huu wa mitandao ya kijamii uliundwa kwa ajili ya watu ambao hata hawawezi kuzungumza kama hawakuwepo,” aliandika.
“Kuna watu ambao wanaogopa kumkaribia mwanamume/mwanamke na kufanya mazungumzo iwe wanataka kuomba namba au kutongoza! Pia alisema huwezi kusema ukweli hapa kwa sababu huu ni ulimwengu wa watu bandia…Watu wanaopenda maisha haya kuliko watu!” Aliongeza rapa Meek Mill akimnukuu JayZ.
Kwa kuzingatia matumizi machache ya Jay kwenye mitandao ya kijamii, haikuwa vigumu kuamini kwamba alichosema Meek ni kweli.
Inasemekana Jay Z alijiunga na Instagram kwa mara ya kwanza Agosti 29,2015, na kupost kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa marehemu Michael Jackson, lakini akaifuta programu hiyo masaa 14 tu baada ya kupata wafuasi 100,000 kwenye mtandao huo.