Kitendo cha kikosi cha Mbeya Kwanza FC kurudisha mabao maawili kwa dakika tano, kimeendelea kumstaajabisha Kocha Mkuu wa Polisi Tanzania FC Malale Hamsini.
Polisi Tanzania FC wakicheza ugenini siku ya Jumatatu (Novemba Mosi), Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ilitangulia kupata mabao mawili kwa sifuri kipindi cha kwanza, lakini wenyeji wao Mbeya Kwanza FC walisawazisha dakika ya ya 49 na 54 kipindi cha pili.
Kocha Malale Hamsini amesema, mpaka sasa anaendelea kufikiria uwezo wa kikosi cha Mbeya Kwanza FC ambao waliuonesha katika mchezo huo, uliomalizika kwa sare ya 2-2.
Hata hivyo Kocha huyo ameipongeza Mbeya Kwanza FC kwa kuweza kurudisha mabao yote mawili ndani ya dakika tano tu, kipindi cha pili dhidi ya timu yake, pia akimsifia kocha wa timu hiyo, Haruna Hererimana kwa mbinu zake bora.
“Niwapongeze wapinzani wetu. Walipambana na kurudisha mabao yote mawili, si jambo rahisi kufungwa mabao mawili na kurudisha yote.”
“Nimpongeze pia kocha wa timu ya Mbeya Kwanza FC kwa mbinu zake kwa sababu kabla wachezaji wangu hawajajua cha kufanya, tayari walikuwa wamerudisha mabao yote na waliposhtuka, wapinzani wetu walikuwa wameshajipanga kuzuia,” amesema Malale.
Sare hiyo ya 2-2 imeifanya Polisi Tanzania FC inayokamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kufikisha alama 10 baada ya kucheza michezo mitano, huku Mbeya Kwanza FC ikifikisha alama 7 na kushika nafasi ya 6, huku ikicheza michezo mitano.