Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 10, Novemba 2021 amefungua warsha ya utafiti ya REPOA ya 25 ,warsha ilioandaliwa kwa kushirikiano na Wizara ya Viwanda na Biashara. Warsha hiyo ya mwaka 2021 limebeba dhima ya Mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uzalishaji viwandani na biashara shindani.
Akifungua Warsha hiyo Makamu wa Rais amesema katika karne ya 21 Taifa haliwezi kupata maendeleo ya haraka pasipo kutumia tafiti kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia mara kwa mara hivyo utoaji maamuzi pamoja na kupanga mipango ya maendeleo kunahitaji kuongozwa na matokeo ya tafiti.
Amesema serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa watafiti wa ndani katika kuwawezesha kuzalisha tafiti za sera zenye ubora pamoja na kuwahusisha katika majadiliano wakati wa utungaji wa sera mbalimbali za taifa.
Aidha Makamu wa Rais ameziasa sekta binafsi kuendelea kutoa mchango wao katika kukuza uchumi shindani ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika kuwejengea uwezo vijana ili kuwawezesha kuwa na ufanisi katika kazi, huku akitoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kutoa mchango wao katika vipaumbele vya taifa pamoja na kuwasihi watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na uwazi ili kuliletea taifa maendeleo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa REPOA Dkt. Donald Mmari amesema warsha hiyo ni muhimu kwa kuwa inatoa nafasi kwa watunga sera na viongozi kusikia matokeo ya tafiti pamoja na uzoefu wa nchi nyingine ili kuhuisha mipango na sera za Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka zaidi.