Mlinda Lango wa klabu ya Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma ameweka wazi kwamba, hajazoea hali ya kushindania nafasi kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyo sasa.
Mlinda Lango huyo kutoka nchini Italia ana wakati mgumu wa kuthibitisha uwezo wake na kuupiku uwezo wa Keylor Navas ambaye amekuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha PSG tangu ajiunge na miamba hiyo ya Ufaransa akitokea Real Madrid.
“Haiathiri kiwango changu, lakini inanisumbua,” Donnarumma aliiambia TNT Sport katika mahojiano kuhusu upinzani wa namba dhidi ya Navas.
“Si rahisi, kwa sababu siku zote nimezoea kuwa namba moja na muda mwingine inauma kukaa benchi.
“Lakini nina hakika jambo hili litamalizwa,” aliongeza.
Donnarumma alisajiliwa PSG, Juni 16 mwaka huu 2021 akitokea AC Milan ya nchini Italia, huku akisaini mkataba wa miaka mitano.