Aliyekua Kocha Mkuu wa Geita Gold FC Ettiene Ndayiragije, ameushukia Uongozi wa Klabu hiyo na kusema haujasema ukweli wa mambo, na badala yake wamedhamiria kumchafua kwa kigezo cha Mkataba.
Ndayiragije ambaye amewahi kuwa Kocha wa Klabu za Mbao FC, KMC FC na Azam FC kabla ya kutimkia Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ aliajiriwa na Geita Gold Sports mwanzoni mwa msimu huu, baada ya klabu hiyo kupanda daraja ikitokea Ligi Daraja la kwanza hadi Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo baada ya michezo minne ya Ligi kuu alisitishiwa ajira yake, kufuatia kikosi cha Geita Gold FC kushindwa kupata matokeo mazuri kwa kigezo cha kutokukidhi sehemu ya mkataba aliousaini wa kumtaka ashinde kila mchezo wa Ligi Kuu.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amefunguka kwa mara ya kwanza na kueleza Kinaga Ubaga cha kipengele cha mkataba ambacho kinadaiwa kuwa chanzo cha kutimuliwa Gaita Gold FC.
Akizungumza kwenye kipindi cha Michezo cha The Score Board kinachorushwa na Radio Times FM, Kocha Ndayiragije amesema suala la kuwepo kwa kipengele cha kushinda kila mchezo wa Ligi Kuu sio la kweli, na limekua likizushwa na viongozi wa klabu ya Geita Gold FC kama sababu.
Amesema ni vigumu kwa mtu yoyote kuamini kama Geita Gold FC inaweza kushinda michezo yote ya Ligi Kuu, kutokana na kikosi chao kukosa sifa hiyo.
“Kuhusu kipengele cha kushinda kila mechi kama ni kweli wangeonyesha kipengele na kama kingekuwepo kwa timu ipi ambayo @geitagoldfc waliyokuwa nayo ya kushinda kila mechi!”
“Moja ya matatizo makubwa ya mpira wa Tanzania ni watu wengi kuwa na matarajio makubwa wakati maandalizi na uwekezeji ni mdogo.” amesema Ettiene Ndayiragije