Mshambuliaji Ditram Nchini amezitaja klabu za Geita Gold FC, Namungo FC na Polisi Tanzania FC kuwa kwenye mpango wa kumsajili kupitia Dirisha Dogo, ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15 mwaka huu.

Nchimbi amezitaja klabu hizo, kufuatia mkataba wake na Young Africans kutarajia kufikia kikomo mwezi Desemba, huku taarifa zikieleza kuwa Uongozi wa klabu hiyo umeshampa mkono wa kwaheri.

Mshambuliaji huyo ambaye aliwahi kutamba na klabu ya Mbeya City, Njombe Mji, Azam FC, Polisi Tanzania kisha Young Africans, amewataka mashabiki wake kuendelea kuwa na subra, kwani muda sio mrefu watafahamu wapi anapoelekea.

“Mkataba wangu na Young Africans SC unakwisha tarehe 15 Decemba 2021 saa 00:00 (saa sita usiku). Kwa sasa nipo likizo mpaka mkataba wangu utakapokwisha ndio maana sipo na timu.”

“Nina ofa nyingi tu mkononi, kutoka Police, Geita, Mtibwa, Namungo na timu nyingine nyingi tu. Baada ya mkataba kwisha mtafahamu naelekea wapi.” amesema Ditram Nchimbi

Hata hivyo siku ya Jumatatu (Novemba 15) Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya young Africans Hassan Bumbuli alinukuliwa na vyombo vya habari akisema: “Ni kweli Ditram Nchimbi mkataba wake unaisha mwezi Ujao tarehe 15, na ndipo dirisha la Usajili dogo litafunguliwa, ndio maana kwa sasa taarifa mbalimbali zinaongea kuhusu yeye sababu kanuni zinamruhusu”

“Kwa sasa yuko nje ya kambi yetu sababu aliomba ruhusa kwenda kwao kutokana na matatizo ya kifamilia, lakini mambo yake yatakapoisha atarejea kambini”

“Tunasubili taarifa ya mwalimu baada ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza FC, itakayoelezea ni wachezaji gani wa kuachwa na wachezaji gani wa kusajiliwa.”

“Kwa hiyo ripoti ya mwalimu ikionyesha anahitaji kuendelea kubaki na Nchimbi tutakaa nae mezani, lakini ikionyesha hamhitaji basi tutamtakia Kila la kheri.”

Tangu kuanza kwa msimu huu 2021/22 Mshambuliaji Ditram Nchimbi hajawahi kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans kilichoshiriki michezo ya Ligi Kuu, huku akiwa chaguo la tatu baada ya Fiston Mayele na Heritier Makambo.

Ndayiragije: Gaita Gold ishinde kila mchezo kwa timu ipi?
Simba SC kuondoka leo Dar es salaam