Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuondoka Jijini Dar es salaam kesho Alhamis (Novemba 18), kuelekea mkoani Lindi tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa sita wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.

Young Africans watakua wageni wa Namungo FC siku ya Jumamosi (Novemba 20), Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda michezo yao mitano iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo Kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati zimeeleza kuwa, Kikosi cha Young Africans na maafisa wa Benchi la Ufundi kilitarajiwa kuondoka Jijini Dar es salaam leo Jumatano (Novemba 17), lakini kuna mabadiliko yaliyofanywa na rasmi kitaondoka kesho Alhamis.

Kabla ya kusimama kwa Ligi Kuu kupicha michezo ya kimataifa (Kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022), Namungo FC walipoteza mchezo dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC kwa kufungwa bao 1-0, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku Young Africans wakiichapa Ruvu Shooting mabao 3-1.

Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 15, huku Namungo FC ikiwa nafasi 11 kwa kuwa na alama 5.

Simba SC kuondoka leo Dar es salaam
Simba SC: Young Africans wanajifurahisha