Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wanatarajia kuanza safari ya kuelekea Jijini Mwanza leo Jumatano (Novemba 17) majira ya jioni, tayari kwa mpambano wa Mzunguuko wa sita wa Ligi Kuu dhidi Ruvu Shooting.

Uwanja wa CCM Kirumba utakua shuhuda wa pambano hilo litakalopigwa keshokutwa Ijumaa (Novemba 19), huku Ruvu Shooting wakiwa wenyeji.

Taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Simba SC imeeleza kuwa: “Kikosi leo jioni kitaondoka jijini Dar es salaam kwenda jijini Mwanza kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting.”

Msimu uliopita Ruvu Shooting waliupeleka mchezo wao dhidi ya Simba SC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza na matokeo yaliwaelemea, baada ya kufungwa mabao 3-0.

Msimu huu 2021-22, Simba SC inayonolewa na Kocha Mpya kutoka nchini Hispania Franco Pablo Martin imeshashuka dimbani mara tano na kuambulia alama 11 zinazoiweka nafasi ya pili kwenye msimamo, huku mchezo wao wa mwisho wakiifunga Namungo FC bao 1-0 katika Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya 10 ikiwa na alama 6, ilipoteza mchezo uliopita kwa kufunga mabao 3-1 dhidi ya Young Africans, inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 15.

Nchimbi: Naondoka Young Africans
Young Africans kuifuata Namungo FC