Kocha Mkuu wa FC Bayern Munich Thomas Tuchel amepotezea taarifa za kuombwa kubaki kwenye klabu hiyo, baada ya kuulizwa swali hilo katika mahojiano maalum aliyofanyiwa na TNT Sports.

Mwezi Februari uongozi wa Bayern ulitangaza utaachana na Tuchel mwishoni mwa msimu huu 2023/24, ikiwa bado ana mwaka mmoja kwenye mkataba wake klabuni hapo, lakini matokeo mabaya na kushindwa kufikia malengo katika Ligi ya ndani imekuwa sababu za kusitishwa kwa mkataba huo.

Hata hivyo Kocha huyo amewafikisha ‘The Bavarians’ hatua ya Nusu Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na baadae leo Jumatano (Mei 09) watakipiga dhidi ya Real Madrid, huku mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliozikutanisha timu hizo ukishuhudia matokeo ya sare ya 2-2.

Tuchel alipoulizwa atakuwa wapi msimu ujao 2024/25, Kocha huyo kutoka nchini Ujerumani alijibu: “Imekuwa bahati kuwa hapa, lakini lazima niseme ukweli, kwa sababu tuna makubaliano, hakuna sababu ya kutilia shaka makubaliano haya kwa sasa. Tumefika hapa kwa kushirikiana na Uongozi pamoja na Wachezaji, lakini sina budi kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

“Sihitaji kulazimishwa kuendelea kuwa hapa, wala mimi sitalazimisha kuwa hapa, kilichobaki kwangu kwa sasa ni kuhakikisha naiacha klabu katika mazingira mazuri, tupo kwenye michuano mikubwa Barani Ulaya, nitahakikisha tunapambana ili tuingie Fainali na ikiwezekana kutwaa Ubingwa wa Ulaya.

“Wapinzani wangu (Real Madrid) wapo vizuri hasa wapokuwa katika hatua kama hii tunayokwenda kukutana nao, lakini mchezo bado upo wazi kila mmoja anaweza kushinda na kusonga mbele.”

Swali lingine aliloulizwa Tuchel ni kama ataweza kurejea Chelsea, lakini alijibu: “Nisingependa kujibu lakini sio siri kwamba niliipenda Chelsea, niliipenda Uingereza na niliipenda Ligi ya EPL kwa hakika, ulikuwa wakati wa kipekee sana na ninaukumbuka vizuri sana.”

Iwapo Bayern watashinda dhidi ya Real Madrid na kutinga hatua ya Fainali itakayochezwa katika Uwanja wa Wembley, Tuchel atakuwa meneja wa pili kuzipeleka timu tatu tofauti katika Fainali ya UEFA Champions League.

Gesi kama Luku: Tafuteni Wataalamu tufanye nao kazi - Rais Samia:
Polisi wamsaka aliyezusha utekaji Watoto 12