Waziri wa Saynsi na Teknolojia Profesa Ndalichako amesema kuwa serikali imeruhuru wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua.
Amesema hayo leo Novemba 24, 2021 wakati akizungumzia mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara ambapo amesema kwa sasa kinachosubiriwa ni waraka ambao atautoa wakati wowote kuanzia leo.
“Hapa zege halilali, nitatoa waraka huo leo na hapa najaribu kutazama karatasi yangu siioni lakini kazi inaendelea leo hii nitatoa ili Watanzania wajue,” amesema Profesa Ndalichako.
Kauli ya Waziri imekuja wakati kukiwa na mjadala mrefu nchini kuhusu wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni wakitaka waendelee na masomo huku wengine wakigoma kwamba utaharibu mfumo wa elimu.
Kuhusu wanafunzi kurudia masomo amesema shule za Msingi walikuwa wamenyimwa haki kwani wenzao wa kidato cha nne na sita walikuwa na nafasi ya kurudia masomo pale wakishindwa kufaulu mitihani.
Hata hivyo amesema utaratibu wa kujifunza utakuwa kwa namna yao binafsi siyo katika mfumo wa Kiserikali kama inavyofanyika kwa vidato vya nne na sita.