Mshambuliaji wa zamani wa klabu za Mtibwa Sugar na Young Africans Said Bahanuzi amesema wachezaji wote wa Simba SC wana nafasi kubwa ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Franco Pablo Martin.

Bahanuzi amesema wachezaji wa Simba SC wana bahati kubwa ya kuwa na Kocha Mkuu mpya mwanzo wa msimu, jambo ambalo linafungua milango kwa wachezaji wote kumshawishi kocha huyo kutoka nchini Hispania.

Amesema mabadiliko ya makocha mara nyingi yanawapandisha baadhi ya wachezaji na wengine kushuka, hivyo ni wajibu wa kila mchezaji wa Mabingwa hao wa Tanzania Bara kuitumia vyema fursa iliopo.

“Pale Simba SC, John Bocco alikuwa anaanza, sasa anaonekana kusubiri mbele ya Kagere, haina maana kwamba Bocco ni mbaya na ndiye kioo cha washambuliaji wa ndani, hii inatafsiri lazima kila mchezaji ajitume kwa nguvu zake zote,”amesema.

Bahanuzi pia akamzungumzia kiungo Ibrahim Ajibu kwa kusema tayari kocha ameanza kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza, anaamini akikaza buti ataacha alama ya heshima msimu huu.

“Msimu ulioisha Ajibu alikuwa hajapata nafasi, kadri msimu huu anavyopata dakika za kucheza zitamrejesha kwenye mstari hadi atakuwa anatumika timu ya Stars,” amesema Bahanuzi.

Kocha Franco Pablo Martin aliajiriwa Simba SC mwezi uliopita, akichukua nafasi ya Kocha kutoka nchini Ufaransa Didier Gomes aliyeshindwa kufikia malengo ya kuipeleka klabu hiyo hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2021/22.

Young Africans yaivutia kasi Simba SC
Majaliwa apiga vita unyanyapaa wa WAVIU