Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umewapongeza viongozi wa Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kwa kukubali kukaa meza moja ili kumaliza tofauti zilizojitokeza wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans Jumamosi (Desemba 11).
Pande hizo tatu ziliingia kwenye mikwaruzano, kufuatia kuzuiwa kuingia uwanjani kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Barbara Gonzalez ambaye anadaiwa alivunja utaratibu wa kuingia eneo la VVIP.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema ni jambo la kufurahisha kuona mamlaka za soka ziko tayari kumaliza mikwaruzano iliyojitokeza, na kuleta taswira tofauti miongoni mwa wadau wa soka.
“Sasa tunakwenda kutafuta suluhu, wamekubali kukaa na kuzungumza, hivyo nawasihi wanachama na mashabiki wa Simba watulie, litafikia muafaka na baada ya vikao vyetu tutatoa ufafanuzi ulionyooka, kwa sasa Wanasimba wajue kuwa viongozi wao wanalishughulikia suala hilo,” amesema Try Again.
Amesema hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Barbara kuzuiwa, kwani hata yeye, na Mshauri wa Mwekezaji wa Klabu ya Simba, Crescentius Magori walikumbana na kadhia hiyo.
Kuhusu ujenzi wa uwanja, Tyr Again amesema watakaa kikao na hivi karibuni watatoa utaratibu wa wanachama kuchangia.
Kuzuiwa kwa Barbara ndiko kulikoibua hisia za mashabiki wa Simba SC kutaka kuchangia ili kuondokana na kadhia hiyo.