Uongozi wa Klabu ya Mtibwa Sugar unatarajia kumtangaza kocha mpya wa atakayerithi mikoba ya Joseph Omog ambaye juzi Jumatatu (Desemba 13) alisitishiwa mkataba wake klabuni hapo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mwasilino ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru, amesema wakati wowote Uongozi utatoka na jina la Kocha Mkuu mpya na kulitangaza hadharani.

Amesema Mchakato wa kumpata Kocha Mkuu mpya wa Mtibwa Sugar umekua mgumu na mzito, kutokana na makocha wengi na wenye hadhi kuwasilisha maombi ya kutaka kuchukua nafasi ya Omog, ambaye ameondoka kufuatia mambo kumuendea kombo.

Kuhusu Kocha Salum Mayanga ambaye imeshathibitiska amevunja mkataba na Tanzania Prisons, kutangazwa kuwa Kocha Mkuu Mtibwa Sugar, Kifaru amesema hawezi kuthibitisha hilo kwa asilimmia 100.

“Kuhusu Mayanga siwezi kuthibitisha hilo, kwani yeye ni muajiriwa wa kiwanda cha Mtibwa na huwa anaruhusiwa tu kwenda kuzinoa timu na mkataba wake ukimalizika huwa anarudi nyumbani,” amesema Kifaru.

“Kwa sasa tunaendelea kuchambua majina ya makocha wa hapa ndani na wengine kutoka nje ya nchi na ndani na siku chache zijazo tutamtangaza rasmi kocha mkuu wa Mtibwa.”

Aidha, amesema Omog ambaye ni raia wa Cameroon wamemalizana naye na leo Jumatano (Desemba 14) ataondoka rasmi nchini kurudi kwao na tayari wameshamkatia tiketi.

Kwa mujibu wa kifaru, Mtibwa sasa inaongozwa kwa muda na Awadh Juma akisaidiana na Shaban Nditi ambaye alikuwa nahodha wa zamani wa timu hiyo.

Mtibwa hadi sasa imepata ushindi mmoja tu katika mechi nane ilizocheza kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na inashika nafasi ya 15 ikiwa na pointi tano.

Simba SC, TFF, TPLB kukaa meza moja
Wataalam kuongezwa daraja la Kigongo- Busisi