Mgombea wa Urais wa Chama cha ODM, Raila Odinga ameweka bayana kuwa hatapuuza uwepo wa Uhuru Kenyatta katika serikali ya Azimio la Umoja iwapo muungano huo utashinda uchaguzi wa Agosti 2022 nchini Kenya.

Akizungumza katika mahojiano na chombo cha habari cha BBC, Jumanne, Machi 15, kiongozi huyo wa ODM alisema Uhuru atakuwa sehemu ya serikali yake kama mshauri wake kwa kuwa ameshirikiana nae hapo awali na kwamba haitakuwa jambo kubwa kumkabidhi majukumu ya serikali.

“Nimefanya kazi na Uhuru Kenyatta hapo awali. Atakuwa mshauri kama vile nilivyokuwa kwake katika utawala wake. Anaweza kuishauri serikali kuhusu masuala ya uchumi au hata kuchukua majukumu ya kidiplomasia kama mimi. Kuna majukumu mengi rais ana uwezo wa kutekeleza,” Raila aliambia BBC.

Ushirikiano wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga umestahimili mtihani wa muda wa miaka minne baada yao kuingia katika mkataba wa maridhiano Raila na Uhuru wakati wa kongamano la Jubilee katika ukumbi wa KICC.

Akikanusha madai kuwa yeye ni mradi wa serikali, Raila alisema kuwa amekuwa na mahusiano mazuri na Uhuru tangu jadi. “Raila hawezi kuwa mradi wa yeyote. Nimefanya kazi na Uhuru, nikiwa Waziri Mkuu alikuwa naibu wangu na tulifanya kazi vizuri,” aliongeza.

Raila alipigia debe mapatano yao na Rais Kenyatta mnamo Machi 2018, akisema kuwa yaliepusha Kenya dhidi ya kusambaratika. “Baada ya uchaguzi wa 2017, nchi ilikuwa inasambaratika. Alikula kiapo nami nikala kiapo changu. Watu walikuwa wanapinga na kuaga dunia lakini baada ya mazungumzo tukakubaliana kwamba Kenya ni kubwa zaidi ya watu wawili,” alidokeza.

Viongozi hao wawili waliokuwa mahasimu wakubwa katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2017, wamedumisha ukaribu wao ambao sasa umefikia kilele cha Raila kuidhinishwa na Uhuru kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2022 nchini Kenya.

Jukumu la Uhuru la kumteua mrithi wake katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, limewafanya baadhi ya watu kudai kuwa bado anataka kuhudumu katika serikali ya Raila kwa kuwa amechukua jukumu kubwa katika siasa za mrithi wake na amembariki waziwazi kiongozi wa ODM kuwania kiti hicho baada yake akitaja sababu ni kutokuwa na imani na ambaye kwa sasa ni naibu wake wa urais William Ruto.

Mulamula amtambua balozi wa Malawi Tanzania
Siri ya Hayati Magufuli na Mafisadi yafichuliwa