Waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya Fastjet PLC nchini Tanzania, wamejitokeza hadharani na kuweka wazi madai yao ambayo wamekuwa wakiyafuatilia kwa kampuni hiyo tangu iache kufanya kazi mwaka 2018 mwishoni.
Yona Msanga na Mamy Katulila waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya Fast Jet, wakizungumza katika mahojiano maalumu na Dar 24 wamesema waliacha kulipwa rasmi mwaka 2019 Januari na wamefatilia kila hatua za kisheria bila mafanikio kutoka kwa mmiliki wa Tanzania wala kampuni mama ya Fastjet.
Kwa naiaba ya wafanyakazi wengine wa Fastjet, wawili hao walifika katika studio za Dar24 na kueleza kuwa pamoja na kupewa mikataba rasmi ya miaka 3 na kampuni hiyo, mabadiliko ya ghafla yalianza kuonekana yaliyowafanya wagundue tatizo mpaka ambapo safari zilisitishwa.
“Hapakua na taarifa maalumu kuwa kampuni imefungwa ila tuliona mabadiliko ya ufanyaji kazi mfano unapangwa siku ya safari unaweka Airport au nyumbani unasubiri tu bila kuelewa muda upi unaenda kazini”, Alisema Mamy ambae alikua mhudumu wa ndani ya ndege hiyo.
“Baada ya Kuona mambo hayaeleweki kuanzia huo mwaka 2019 Januari, tulifuata taratibu za kisheria kuanzia TCAA na wakatushauri tufungue kesi na kuwashitaki wamiliki ambao ni Fastjet PLC kampuni mama na Fastjet Tanzania ambae mmiliki ni Laurence Masha na kesi ilikua ya madai na zuio kwa ndege”, aliongeza Mamy.
Taarifa za awali zinasema kuwa ndege aina ya ‘5H-FJH-Embraer E190AR’ mali ya kampuni ya Fastjet imefutiwa usajili wa kufanya kazi hapa nchini Tanzania mwanzoni mwa mwaka huu 2022 na taarifa zinasema kuwa inaweza kuondolewa nchini Tanzania wakati wowote.
“Kilichotushtua sasa ni kuwa ndege hiyo tuliyoizuia wakati tunashughulikia kesi hizo imefutiwa usajili Tanzania maana yake inaweza kuondoka Tanzania mda wowote, na hatukua tumekaa, tulikua tunahangaika, tunatafuta ushauri maana yake haki yetu inapotea”, alisema Mamy.
Katika mazungumzo zaidi Mamy alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ilishirikiana na wafanyakazi hao wa Fastjet kwa kuwa kwa pamoja walikuwa wanaidai kampuni hiyo lakini baadae TRA walilipwa pesa zao na wakajitoa katika zuio la ndege hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Paschal Katambi, alipopigiwa simu na kuzungumzia swala hilo la madai ya wafanyakazi wa Fastjet amesema kuwa suala hilo halifahamu tangu aingie katika Wizara hiyo, ingawa katika majibu zaidi amewashauri wadai hao kuendelea na na taratibu za kiofisi katika Wizara yake ili kuendelea kulifuatilia.
“Sasa mimi nataka niwaambie, mjikusanye na mlilete hili suala kama ‘formal’ kiofisi kwa barua sio kwamba tumezungumza hapa kwa simu useme umeshaongea na Naibu Waziri, yani mkae kikao, kwa majina na sahihi, na muelezee kila hatua mliyopitia na kila mmoja anaandika deni lake, na hapo sasa sisi tunakua na mamlaka kwa sababu kuna madai rasmi tumeyapokea”, alisema Katambi.
Naibu Waziri Katambi ameonesha nia ya kuwasaidia wafanyakazi hao kwa kukutana nao na kupokea nyaraka zote husika, na atakapofanikiwa kupata vigezo vyote atashirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani katika zuio la ndege hiyo mpaka madai ya wafanyakazi hao yatakaposhughulikiwa.
Takribani wafanyakazi 105 waliokuwa kwenye kampuni ya FastJet wanadai maslahi yao ambayo hawakuwa wamepewa wakati kampuni hiyo ikiacha kufanya kazi hapa nchini Tanzania tangu mwaka 2018 mwishoni na mara ya mwisho kulipwa stahiki zao ilikua Januari 2019.