Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewapongeza waandamanaji katika mji unaokaliwa kimabavu wa Kherson, kwa ujasiri wao wa kukabiliana na wanajeshi wa Urusi waliofyatua risasi kutawanya maandamano hayo.

Akizungumza kwa njia ya video, Zelensky amesema wameona “watumwa wakifyatua risasi kwa watu walio huru na kuwataja wanajeshi wa Urusi kama watumwa wa propaganda.”

Rais huyo wa Ukraine ameongeza kuwa, vita hivyo vimewageuza raia wa kawaida wa Ukraine kuwa mashujaa na kwamba ushujaa huo pia umewashangaza maadui.

Wanajeshi wa Urusi jana Jumatatu walitumia mabomu na kufyatua risasi hewani ili kuzima maandamano katika mji wa kusini wa Kherson. Waandamanaji hao wanapinga hatua ya kuchukuliwa kwa nguvu mji huo wa kusini mwa Ukraine baada ya uvamizi wa mwezi uliopita.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alichapisha video kwenye mtandao wa Twitter, ikimuonyesha mwanamume aliyebeba bendera ya Ukraine aliyejeruhiwa kwa risasi. Kwenye video hiyo, milio ya risasi inasikika na kuonyesha watu waliobeba bendera wakikimbia ili kumsaidia mwanamume huyo aliyekuwa akivuja damu.

Kherson, mji wenye takriban watu 200,000 upo karibu na rasi ya Crimea, iliyotwaliwa na Urusi mwaka 2014 na ni mojawapo ya njia zilizotumika na Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi uliopita.

Mji huo ulikuwa wa kwanza kuingia mikononi mwa vikosi vya usalama vya Urusi, huku Moscow ukiuteka mji huo ndani ya wiki ya kwanza ya uvamizi wake nchini Ukraine. Watu wa mji huo hata hivyo wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara kupinga kuchukuliwa kwa nguvu mji huo wa kusini.

Vyombo vya habari nchini Ukraine vimeripoti mara kadhaa kuwa vikosi vya usalama vya Urusi vimekuwa vikiwafyatulia risasi waandamanaji.

Mpango wa Maendeleo ya Kilimo Afrika kujadiliwa
Wakuu wa upelelezi wapewa maagizo